MAFIA ISLAND TANZANIA image branding - people of Mafia Island

Nyumbani

Akiolojia na Historia

Idadi ya watu na sensa

Ikiolojia (pamoja na Hifadhi ya Bahari)

Uchumi

Utalii

Afya na miradi ya afya

Vyama hiari

Habari mbalimbali za Kisiwa cha Mafia

Picha za Mafia

English Home

Kisiwa cha Mafia: Ukurasa wa Orodha

Kisiwa cha Mafia kipo karibu na mlango wa Mto Rufiji kusini mwa Tanzania. Ni miongoni mwa maeneo yaliyo nyuma zaidi kimaendeleo kwenye nchi masikini ya Tanzania, hata hivyo, kimekuwa na kinaendelea kuwa sehemu muhimu ya mabadiliko ya kihistoria. Ingawaje maeneo ya kuvutia ya mazingira ya bahari yametokea kujulikana zaidi haswa mara baada ya kuanzishwa Hifadhi ya Bahari (Mafia Island Marine Park - MIMP) na Maeneo Tengefu, habari nyenginezo zimekuwa adimu kupatikana. Unapotafuta habari za Kisiwa cha Mafia kwenye mitandao kunapelekea kupata taarifa za vivutio vya utalii pekee ambavyo vinajenga sura ya kisiwa hiki kuwa ni pepo ya watalii (angalia mtandao wa utalii) miongoni mwao hawatoi picha sahihi ya mambo yalivyo.

Hali ya miundombinu kisiwani Mafia ni duni: umeme unapatikana makao makuu ya wilaya na maeneo ya utalii ya Utende pekee. Kuna nyumba chache zenye maji ya bomba. Usafiri kwenda kisiwani hapo ni aidha kwa ndege ndogo kutokea Dar es Salaam ambazo aghalabu ni juu ya uwezo wa wakazi wengi wa kisiwani, au kwa mashua kupitia Kisiju na baadaye kulazimika kupanda lori au basi hadi Dar es Salaam. Safari za mashua mara nyingi huchukua muda mrefu, zenye hatari na misukosuko lakini ndiyo njia pekee ambazo wakazi waliowengi wa Kisiwa cha Mafia hulazimika kutumia. Barabara chache kisiwani hapo zipo katika hali mbaya na vyombo vya usafiri wa barabarani ni vichache. Hivyo wengi hutumia baiskeli au kwenda kwa miguu. Mawasiliano ya simu hadi hivi karibuni yalikuwa yanategemea simu za upepo kuunganisha bara na kisiwa cha Mafia. Wakati kila kijiji kina shule yake ya msingi, shule ya sekondari ni moja tu na nyengineyo iko mbioni kukamilika

Wakazi walio wengi wa Kisiwa cha Mafia ni masikini wa kupindukia. Zao kuu la nazi, limepungua bei kwenye masoko ya nje na ya ndani (Angalia mtandao wa Uchumi). Kisiwa cha Mafia ni miongoni mwa sehemu zilizokumbwa na ukame wa takribani miaka mitatu, wakati shughuli za uvuvi ambazo zimeanza kuleta tija katika miaka ya hivi karibuni, zimekuwa zikifanyika katika maeneo maalumu ya kusini zinazopakana na Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (angalia Ukurasa wa Ikolojia).

Kisiwa cha Mafia hakina gazeti, duka la vitabu, au maktaba yake, watu hutegemea njia ya mawasiliano ya radio kupata habari za ulimwenguni. Hata hivyo, mawasiliano ya kisasa ya televisheni kwa njia ya setelaiti yameanza kupatikana kisiwani hapo. Huduma za simu za mkononi zimeanza kisiwani hapo ingawa ni kwa wachache wenye uwezo hususani, wale watumishi wengine wa serikali. Mwaka 2004, Kisiwa cha Mafia kimepata huduma za intaneti kutumia teknolojia ya setilaiti. Moja ya huduma hizo ipo makao makuu ya wilaya (Kilindoni) na ngineyo ipo katika maeneo ya utalii ya Utende. Huu ni mwanzo wa hatua zitakazopelekea wenyeji kutumia huduma za email na hata intaneti ili kupatia habari. Hii itasaidia wenyeji waweze kupata habari za kisiwa chao. Nimatumaini yangu kuwa tovuti hii itatumiwa na watu waliomo katika njanja mbalimbali, hususan:
  • Wanafunzi wa sekondari wanaotaka kupata habari zaidi za kisiwa chao
  • Watumishi wa serikali wanaoshughulikia sera na mipango ya maendeleo ya wilaya
  • Watanzania wanaotaka kujua habari za sehemu ya nchi ambayo habari zake hazijulikani
  • Mashirika ya misaada na miradi iliyopo katika maeneo ya kisiwani hapo
  • Walimu wazawa na wageni wanaofanya utafiti wa Kisiwa cha Mafia na maeneo yanayokaribiana
Ninakaribisha maoni na mapendekezo ya ziada ilikujaliza tovuti hii na kuiboresha zaidi. Matazamio ya baadaye nikuongezea habari zaidi kwa Kiswahili na kuweka ukurasa wa kutolea maoni na mijadala ihusuyo Kisiwa cha Mafia na njia madhubuti za kuiendeleza. Tafadhali wasiliana nami kutumia email ifuatayo: p.caplan@gold.ac.uk1

Habari Zangu Binafsi
Kwa mara ya kwanza nilikiona kisiwa cha Kisiwa cha Mafia mnamo mwaka 1962 wakati nikisafiri kwa stima ndogo ya Kiitaliano kutokea Kilwa Kisiwani kuelekea Mombasa. Miaka mitatu baadaye nilirejea kufanya utafiti wangu kama sehemu ya Tasnifu ya Ph.D. Tangia hapo nimekuwa nikirudi mara kwa mara kisiwani hapo ambapo safari yangu ya mwisho ilikuwa majira ya kiangazi mnamo mwaka 2004 (unaweza kubonyeza hapa kuona orodha yangu ya machapisho yahusuyo kisiwa hiki na kuangalia website yangu binafsi www.goldsmiths.ac.uk/departments/anthropology/staff/pat-caplan).

Katika ziara yangu ya 2002, niliombwa na watu kadhaa kuandika yanayohusu Kisiwa cha Mafia na Watanzania kwa ujumla. Wazo langu la kwanza lilikuwa kushirikiana kuandika kitabu pamoja na rafiki, kaka yangu wakufikia, na msaidizi wangu Mikidadi Juma Kichange. Kwa bahati mbaya, Mikidadi alifariki ghafla mara baada ya ziara yangu ya 2002. Hivyo nikaamua kuwa tovuti hii itakuwa njia maridhawa kwa kuyaandikia habari za Kisiwa cha Mafia na wengi niliozungumza nao juu ya wazo hili walioyesha shauku na kuliunga mkono wazo hilo.

Picha zote nimepiga mwenyewe, ila Chris Walley amepiga ukanda wa sinema wa Zahanti ya Chole. Namshukuru kunipa ruhusu kuzitumia.

Shukrani zangu za dhati kwa Nuffield Foundation ambao walifadhili utafiti wangu wa Kisiwa cha Mafia, na vile vile kukubali kuidhamini tovuti hii. Na shukrani ziwaendee vilevile Chuo cha Goldsmiths ambapo nilikuwa nikifundisha somo la anthropolojia-jamii (bonyeza mtandao wa idara yangu) kwa miaka 25 sasa kwa kukubali kuipa nafasi tovuti hii. Na shukrani vilevile kwa Dan Watson ambaye alifanya kazi ya kuwekea saiti hiyo na Ahmed Kipacha kwa kutafsiri kutoka Kiingereza.

Shukrani zangu za dhati kwa Nuffield Foundation ambao walifadhili utafiti wangu wa Kisiwa cha Mafia, na vile vile kukubali kuidhamini tovuti hii. Na shukrani ziwaendee vilevile Chuo cha Goldsmiths ambapo nilikuwa nikifundisha somo la anthropolojia-jamii (bonyeza mtandao wa idara yangu) kwa miaka 25 sasa kwa kukubali kuipa nafasi tovuti hii. Na shukrani vilevile kwa Dan Watson ambaye alifanya kazi ya kuwekea saiti hiyo na Ahmed Kipacha kwa kutafsiri kutoka Kiingereza.

PC, Octoba 2004.